Podcasts · Neno la Leo

Kisasi Hakiponyi Jeraha!

· 10 min · S4 E9

Episode Kisasi Hakiponyi Jeraha!

0:00 10:13

🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

Leo kupitia 2 Samweli 13:28–29 tunaendelea na simulizi ya familia ya Daudi, ambako maumivu ambayo hayajashughulikiwa sasa yanazaa maumivu mengine.

Jana tulimwona Absalomu akiwa amebeba hasira na chuki dhidi ya Amnoni baada ya kile alichomfanyia dada yake Tamari.

Leo tunagundua jambo muhimu:

Miaka miwili imepita, lakini hasira ya Absalomu haijaisha.

Kwa nje alikuwa kimya. Lakini ndani yake alikuwa amebeba mpango wa kulipiza kisasi.

Hatimaye, Absalomu anaandaa mazingira na kuwaamuru watumishi wake wamuue Amnoni.

Huenda kwa mtazamo wake alikuwa analipiza uovu uliofanywa dhidi ya Tamari.

Lakini angalia kilichotokea.

Tamari aliumizwa. Absalomu akajawa na chuki. Amnoni akauawa. Na familia ikaendelea kuvunjika.

Uovu wa kwanza haukurekebishwa kwa kuongeza uovu mwingine.

Na hapa ndipo tunapata somo kubwa:

Kisasi kinaweza kumuumiza aliyekuumiza, lakini hakiwezi kuhakikisha kwamba jeraha lako limepona.

Wakati mwingine tunapoumizwa, tunaanza kufikiri kwamba tutapata amani siku ambayo aliyetuudhi ataumia kama tulivyoumia.

Tunasema moyoni:

“Atajua nilivyojisikia.”

“Nitamuonyesha.”

“Hawezi kunifanyia hivi halafu akaendelea na maisha yake.”

Lakini swali ni hili:

Baada ya kulipiza kisasi, je, maumivu yako yatakuwa yamepona?

Warumi 12:19 inatukumbusha tusijilipize kisasi. Na Yesu katika Mathayo 5:44 anatufundisha kuwaombea hata wale wanaotutendea mabaya.

Hii haimaanishi kwamba tunapaswa kupuuza uovu.

Haimaanishi kwamba mtu aliyedhulumiwa anapaswa kunyamaza.

Na haimaanishi kwamba msamaha unafuta uwajibikaji.

Justice na revenge si kitu kilekile.

Haki hutafuta kushughulikia uovu, kumlinda aliyeumizwa na kuhakikisha uwajibikaji.

Kisasi hutafuta kumfanya mwingine aumie kwa sababu mimi niliumia.

Na tofauti hiyo ni muhimu sana.

Tunaweza kutafuta haki bila kuruhusu chuki ituongoze.

Tunaweza kuweka mipaka bila kupanga kumuumiza mwingine.

Tunaweza kudai uwajibikaji bila kugeuza maumivu yetu kuwa sababu ya kutenda uovu.

Simulizi ya Absalomu inatukumbusha pia kwamba muda peke yake hauponyi kila jeraha.

Miaka miwili ilipita lakini chuki yake iliendelea kukua.

Hata leo, unaweza kuwa umeumizwa miaka mingi iliyopita lakini bado ukabeba hasira ileile.

Ndiyo maana tunahitaji kushughulikia maumivu yetu kwa njia salama na zenye kujenga, kwa kutafuta msaada, haki na uponyaji badala ya kuyalisha mpaka yageuke kisasi.

Na labda swali letu la leo ni hili:

Je, ninatafuta haki au ninatafuta kumuumiza mtu kwa sababu aliniumiza?

Usiruhusu kile mtu mwingine alichokufanyia kiamue wewe utakuwa mtu wa aina gani.

Usiruhusu uovu wake uzalishe uovu mwingine kupitia wewe.

Kwa sababu mwisho wa siku:

Kisasi hakiponyi jeraha. Mara nyingi kinaongeza jeraha jingine.

Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

The episode on the publisher’s site (opens in a new tab)

Shows are listed from Apple Podcasts' charts and directory, and Podcast Index where it is used. Every show and episode belongs to its publisher and plays from the publisher's own feed; this site hosts none of them. Explicit shows are for adult profiles only, and children’s profiles hear only children’s shows. More about this list.